sera za lugha zinazotakikana kanisani, Afrika.

Siku moja nikiwa Zambia, nilipokuwa mwalimu wa shule ya upili, niliweka tangazo fulani kwa sehemu ya taarifa za shule. Baada ya siku mbili nilipitia hapo na Walimu wenzangu Wazambia wawili.  Niliona mtu mwingine alishafunika karatasi yangu kwa kuweka karatasi yake juu ya yangu.  Nilivyowaelezea wenzangu, wakacheka.  Nilifikiri – kwa nini wanacheka kwa kitendo kibaya kama kile?  Niligundua kwamba hata ukitumia lugha moja, bado jinsi inatumiwa inaweza kuwa tofauti. (Kwetu Ulaya mtu hangalicheka, angalisema pole na jinsi inatakikana hali irekebishwe.)

Nilipofika Zambia mara ya kwanza, nikaanza miradi mbali mbali ya ukulima hapo shuleni. Wazambia wenzangu walifurahie kuona maendeleo shambani.  Lakini pia ilionekana kwa ufahamu wao ya kwamba miradi itaendeleo tu nikiwepo au Mzungu mwingine akija kuiendeleza.  Nilianza kuona hio dalili mahali popote nilipoenda.  Nilitafuta piki piki ili nitembee nifanye uchunguzi zaidi.  Sio miradi yangu midogo shuleni tu, lakini miradi mikubwa katika sehemu mbali-mbali ilikuwa inafanya kwa muda kidogo, lakini Wazungu walipoondoka miradi ikaanguka.  Kufungwa kwa miradi yote hapa KIST mwaka uliopita (2005) inaonyesha hali ile ile ngumu pia hapa Kenya.

 

Watu hupenda kutoa sababu mbali mbali kueleza kutofaulu kwa miradi. Wengine husema ni ukosefu wa rasilmali. Huu ni ngumu kuamini vile pesa nyingi imemwagwa kwa bara ya Afrika na shirika mbali mbali za misaada.  Wengine hutaja bahati mbaya, ufisadi, vifo vingi, hali ya hewa, kuwepo vita, ukosefu ya elimu n.k.  Lakini sababu aina hizo kweli zinaharibu hii miradi yote? Hali ingine ya msingi inajificha na maneno aina hayo. Kwa nini miradi ya kuendeleza uchumi wa Kiafrika mara nyingi inakwama?

Tuangalie upande wa kanisa.  Siku moja nilipokuwa Zambia niliambiwa ‘Mwafrika hawezi kuhubiri vile Mzungu anayehubiri.’  Baada ya miaka kadhaa nilipokuwa Kenya niliambiwa ‘Mzungu hawezi kuhubiri kama Mwafrika.’  Nilipuuza kwanza.  Inawezekanaje Mungu kutofanya kwa njia sawa na hawa wote?  Baada ya muda hapa Kenya, nilitambua ni kweli.  Pengine sio haiwezekani kabisa, lakini ni ngumu sana. Tena inafanywa kupitia kwa uigaji. Nimeona pia Mwafrika akienda kuhubiri Ulaya. Waingereza hushangaa kwa urahisi; sio rahisi kuyafahamu maneno yake. Hapa Afrika mara nyingi Watu wanakuwa tayari kulisikiliza Neno la Mzungu ikiwa Mhubiri anatumia lugha ya pesa. Pesa isipokuwepo kugawanya wakati ule anapohubiri, lazima asisitize maneno yake kupitia kwa mali yake kwa njia ngine. Wacha ajaribu kazi yake bila ugawanyaji ya fedha na bila kutumia lugha ya ugeni ambayo inataminikwa, na tuone.

Badala ya kusaidia, mara kwa mara mhubiri mgeni Mzungu analeta vita na ugawanyiko kanisani.  Anawapa watu uamuzi ngumu – fuata Mungu na umaskini, au tii maneno yake na pokea mali.  Haya yamewaangusha watumishi wengi wa ukweli wa Mungu.  Huo ni uharibifu moja unaotokea tukimruhusu mgeni kutumia mali yake kulazimisha maneno ambayo hayalingani na mila inayolengwa.

 

Mara nyingi nimejikuta katikati ya shida hii.  Maana yake; mgeni kutoka Ulaya anaongea na kiongozi wa kanisa hapa Kenya, nikiwa ninasikia.  Mgeni huyu Mzungu anavyoongea, ninayafahamu shabaha yake sababu mimi pia nimetoka mahali ametoka.  Ninagundua pia vile Mwafrika akimsikia anakosa kumfahamu barabara.  Halafu Mwafrika akiongea (tuseme anatumia Kiingereza pia) ninaweza fahamu kitu anacholenga zaidi ya huyu Mzungu sababu nimeishi hapa kwa miaka nyingi.  Lakini jibu la Mzungu linaonyesha kukosa kufahamu kwake.  Hivyo ndivyo mijadala inaendelea.

Ubaya ni; sio rahisi kuwasaidia hawa watu wawili. Kuwaambia hawasikilizani barabara ni kuwakwaza.  Mwafrika anaogopa kupotezwa kwa pesa ambayo anatarajia.  Mzungu hawezi kubali hali ya kuwa mjinga na kutoweza kumwelewa mtu ambaye anatumia lugha yake (yaani Kiingereza).

 

Ninaweza toa mifano jinsi ufahamu unakosekana.  Mwafrika akisema mkutano wa kesho yake utakuwa saa mbili, inafaa Mzungu aambiwe ‘10.00am’ na siyo ‘8.00am’.  Mwafrika akisema ‘nitakuja kesho’ inatakikana Mzungu aambiwe ‘pengine nitakuja kesho.’  Mwafrika akisema ‘tunayo shule za Biblia’ inafaa Mzungu aambiwe ‘tunataka utujengea shule ya Biblia’ (au hospitali, nyumba ya kutunza na kulea yatima, miradi n.k.).

Kujaribu kutatua kwa nini watu wawili wanaotumia lugha moja hawawezi kusikilizana barabara, kilinifanye nitafute kitabu juu ya semantiksi.  Hio nilifahamu ilikuwa masomo juu ya jinsi maneno yanakuwa yanamaanisha kitu.  Nilishangaa kwa ugumu wa kuhakikishia maana ya neno fulani.  Kusema ‘majani ni mabichi’ ni sawa ikiwa ‘majani ni mabichi’ anasema Kempson (1973:24). Kumbe semantiksi peke yake haielezi maana!  Kempson alinielekeza kwa masomo ambayo wakati ule wa 1973 yalikuwa bado mpya, yaani ya isimu amali.

Kuchunguza isimu amali kulinisaidia kufahamu jinsi maana yanatokea kwa kiasi kubwa kwa mazingira na hali ya utumizi wa neno fulani.  Kwa mfano, nikisema ‘leta nguo’ ninaweza maanisha: a/ Ninasikia baridi. b/ Ile nguo ni yangu. c/ Ninataka kukuwekea hiyo nguo. d/ Ninataka ubaki uji. n.k. n.k.  Hayo maneno ‘leta nguo’ yanaweza kuwa na maana nyingi sana kushinda kuhesabiwa.  Kila mara mazingira na mbinu wa utumizi wa maneno inageusha hivyo ndivyo maana ya hayo maneno.

Hii ni sababu Mwingereza anafahamiana na Mwingereza mwenzake kwa kiasi ambacho anakuwa sawa kwa mazingira au ufahamu wa msingi wa maneno yake.  Mwingereza akiongea anaongea akidhania mazingira na historia fulani katika kila neno analotaja.  Ataweza kuwafahamisha tu wengine kwa kiasi ambacho hawa pia wanayafahamu mazingira ambayo anakuwa nayo mawazoni (kichwani) akiongea.  Hivyo ndivyo pia kwa Mwafrika anayeongea. Asipojua vile mazingira na asili ya hayo maneno inakuwa, mtu hataweza kuyafahamu maneno.  Hivyo ndivyo tunaweza sema ukalimani hauwezekani.

Hauwezekani pengine sababu hamna maneno kwa lugha inayolengwa. Nikisema ‘I threw the paper into the bin’ inaweza kuwa ‘nilitupa karatasi kikapuni’, lakini ukweli ni kikapu na bin ni vitu tofauti. Lakini kutowezekana mara nyingi unatokea kwa hali ya isimu amali. ‘Mtu ambaye anaambiwa “njoo hapa haraka’ kwa barabara atahitaji kujua ni nani anamwita kabla hajaitika. Akiwa mzee anayeambiwa hivyo tutashangaa wote, lakini akiwa mtoto mdogo hatutastuka kwa maneno hayo. ‘Nilienda Kisumu kwa gari’ ikitamukwa na mtu ambaye hana mali nyingi, tunafahamu alichukua matatu. Tajiri akisema hayo hayo maneno, tutajua alienda na gari ya binafsi. Utafauti hayo sio kwa maneno, lakini ni nje ya maneno, na kuyatafsiri maneno hakitauelezea.

Kufahamu vile ukalimani unavyobadilisha maana ni muhimu sana ili uhusiano kati ya watu wa mataifa (mila) mbali mbali utawezalainishwa; ikiwezekana!  Mifano itafafanua zaidi. … Kuleta mifano lakini ni ngumu sababu wengi wetu kwa muda mrefu (au maisha yetu mzima) tunakuwa pamoja na watu wa mila fulani moja.  Mtu anagundua utofauti wa ndani ya utumizi wa lugha akiweza kuifahamu mila mbili.  Wengi wetu hatuna hiyo nafasi.  Niruhusu kujaribu kueleza kulingana na mazoezi yangu.

Maneno ya kusema “nimejenga nyumba nzuri” hayatoshi kufahamu vile nyumba yenyewe inayokuwa. Nyumba ya matope moja inaweza kuwa nzuri kuliko nyumba ingine ya matope. Mweskimo akisema amejenga nyumba nzuri, nyumba yake inatengenezwa na barafu. Mfanya biashara penye mji wa New York akisema atajenga nyumba nzuri inaweza kuwa ghorofa ya juu kabisa, sababu New York ni mji wenye magorofa ya juu. Kwa hivyo maana ya hayo maneno “nyumba nzuri” yanategemea mazingira ya utumizi wa maneno.

Swali linakuja sasa kwa elimu kwa jumla.  Kinakuwaje elimu ikitolewa nchi moja na kupelekwa sehemu nyingine pasipo na mazingira na mila ambayo imetegemea kule mahali pa asili?  Mfano ninaweza kuchukua ni elimu ya Uingereza na ya Amerika.  Nimewasikia Waingereza wengi ambao wanasema elimu ya Amerika haifai kwao na Waamerika wengi ninadani wanahesabu elimu yao kuwa nzuri kulikwo hiyo ya Uingereza.  Ikiwa utofauti unaonekana hivi kati ya nchi mbili wenye asili na lugha moja, itakuwaje kuhamisha elimu hiyo kwa watu wenye asili (na lugha) tofauti sana?

Kuifahamisha elimu hiyo kutoka kwa watu na mila moja hati kwa watu wa mila na lugha tofauti ni kuifanya elimu ibaki bila mizizi.  Vile baisikile bila gurudumu haitembei.  Vile mti bila mizizi unakauka haraka sana.  Vile kichwa cha mtu pasipo mwili wake ni bure kabisa.  Vile nyundo bila mpini wa kugusa inakuwa na faida kidogo sana, n.k.

Tufikirie juu ya Mungu.  Watu hufahamuje Mungu?  Tuseme pengine Waafrika wanamfahamu akiwa kama nguvu ambayo ina patikana kupitia kwa vitu vingi (k.m. miti, milima, mito n.k.), au hata kila kitu.  Hiyo nguvu ambayo ni Mungu inayo uhusiano wa karibu na mioyo ya wafu, pamoja na mioyo ya wenye hai.  Tuseme tena Wazungu wanamwamini Mungu akiwa kama Mzee mkongwe ambaye anakaa sehemu za mbingu na ambaye sasa amechoka.  Lakini vile watu siku hizi wanafanya na komputa, huyu Mungu wa Mwingereza ameitengeneza dunia ili ikimbie ‘peke yake.’  Tofauti na hizi mbili tuseme ukweli ni katikati – Mungu sio kitu kimoja na dunia, na uhusiano wake na mioyo ya watu na wafu sio karibu kwa kiasi ambacho Waafrika wanaamini.  Lakini anahusika na mambo ya kila siku duniani zaidi na vile Wazungu wangetuamini.  Basi tunaona mafundisho yanayofaa kwa Mwafrika ili amfahamu Mungu ni kueleza utofauti ya Mungu na dunia, lakini Waingereza wanafaa kufundishwa juu ya hali ya karibu ya Mungu (Mungu yuko karibu nawe)!  Kuchanganya hao wawili (km. kumsisitizia Mwafrika vile Mungu ni kama upepo ambao unakuwa kila mahali au kumsisitizia Mzungu vile Mungu hana nguvu kumtajirisha mtu) sio kusaidia ila kupoteza wasikilizaji.

Tunaona juu ya vile, ikiwa Mungu ni mmoja, na desturi na hali ya maisha yake ni mmoja, watu ambao wako tofauti lazima wafundishwe kwa njia tofauti.

Pikta 1.  Jinsi mafundisho juu ya Mungu yanatakikana kuwa tofauti tukimlinganisha Mwafrika na Mwingerezagt;

 

Tumeona juu ya vile neno moja linaweza kuwa na maana nyingi ya aina mbali mbali.  Kwa ukweli – maana ya neno ni utumizi wake! (Wittgenstein 1989: 42). Maana ambayo neno linaweza kuwa nayo lenye kamusi ni chache tu ukilinganisha na nguvu nyingi aina mbali mbali ambayo inafuruta ‘maana ya utumizi’ wa neno huko na pale.  Sababu maana ya neno, hata sentensi, fungu la maneno (paragraph) au hata kitabu inabadilika kulingana na mazingira na utumizi wake, mafundisho juu ya Mungu au hata mambo mengine kutoka mbali yanaweza kubadilishwa kabisa na kuhamishwa.

Wazungu wengi siku hizi hawaongee hata juu ya imani yao kwa Mungu. Wengine wanasema hawamwamini Mungu.  Hiyo hali ya kushangaza inatokeaje na inadumishwaje?  Kwa ukweli, Waingereza wanayo ‘mungu’ mwingine lakini hawamwite mungu!  Ila, wanamwita (au wanaiita sababu hawaamini hata yuko hai) objectivity.  Nilikuja kwa Bara ya Afrika kwanza miaka kumi na nane iliopita. Wakati ule nilijaribu sana kuwafundisha Waafrika (Wazambia) juu ya huyu ‘mungu’.  Lakini, sababu hakuna mungu ambaye alikuwa anafanana naye kwa tamaduni yao, sikuweza kuwafafanulia.  Lakini huyu mungu anashika sehemu kubwa mno kwa maisha ya Waingereza, mpaka maisha yote yanaelekezwa kulingana na mahitaji yake.  Hata wale wanaomwamini Mungu (tuseme Yahweh) wanamlinganisha (au tafautisha) kila mara na huyu mungu mwingine; objectivity.  Kwa hivyo, haiwezekani kumfahamu vizuri Mwingereza na kufahamu vizuri theologia ya Waingereza pasipo kumfahamu kwanza huyu mungu ambaye anaitwa objectivity, kitu ambacho kwa ufahamu wangu ni ngumu sana au hata haiwezekani kwa Waafrika kwa ujumla sababu mila yao haina kitu kama hicho!

Hiyo ni muhimu sana.  Mara nyingi wasomi, hata wakiwa Waafrika wenyewe, wanachunguza sana mila na kitamaduni yao, hata wakitumia Kiingereza.  Wengi hawajali kujiuliza kwanza – lakini mizizi ya lugha ya Kiingereza ambayo tunaitumia kila mara, inakuwaje?

Tofauti na Waingereza, Waafrika wanaamini kukuwepo kila mara na kila mahali wasikilizaje na waonaji wa vitendo na mazungumzo yao, ambao ni wafu (walioaga).  Kwa majina mengine mapepo, majini, masaitani, mizimu, demons, spirits, nguvu za giza n.k.  Inamchukua Mwingereza muda mrefu kugundua hali hiyo kwa Waafrika wenzake.  Hata wakimwambia ni hivyo, hawezi kubali haraka sababu ni kitu chenye ugeni kwake kabisa.  Kuwepo kwa hawa mapepo kunamfanya Mwafrika kufikiria sana kwanza kabla hajataja maneno fulani, ikiwa kusikia maneno kwa hawa mapepo kunaweza kumdhuru kwa njia yo yote maishani mwake.  Hapa tunayo asili ingine ambayo inafanya kusikilizana na kufahamiana kati ya Waingereza na Waafrika kuwa ngumu sana. Hiyo pia inaonyehsa vile ukalimani hauwezakani.

Hitimisho

  1. Kiingereza kweli inawezakana iwe lugha ya Kiafrika.  Lakini, shida kubwa sana wakati huu kwa nchi kama za Kenya ni vile hairuhusiwe kubadilisha ili iwe lugha ya Afrika.  Badala yake watu wanataka kuitumia Kiingereza ya Ulaya, na hiyo haiwezekani. Kwa hivyo utumizi wa Kiingereza hapa Kenya (Afrika) kwa theologia unaleta uchanganyiko.  Hatua moja kubwa muhimu ili kanisa la Waafrika liendelea ni kuwacha kuitumia Kiingereza au lugha na hali ya ugeni kiasi kama hiyo kama lugha rasmi yake. (Inaweza kuendelea kufundishwa, lakini isiwe lugha ambayo inatumiwa kufundisha, kuongoza ibada n.k.)
  1. Ukalimani sio kazi inaofaa kwa watu wote – k.m. watoto shuleni (ambao siku hizi wanakutana na Kiingereza yenye asili ya ugeni kabisa kwa vitabu vyao na kutoka kwa walimu wao).  Watu waerevu (wasomi) ambao wanayafahamu mila ya Kiingereza na ya Afrika wanahitajika watafsiri maarifa kutoka nje ili yaweza kuwafaidi raia wa kawaida.

 

  1. Ukalimani bado utakuwa ugeukaji. Maarifa kutoka sehemu mbali mbali duniani kweli yanaweza kutusaidia hapa Afrika, lakini haifai kuwekwa msingi wa elimu au maisha yetu.  Lazima msingi ujengwe kwa Mungu, kupitia lugha yetu na mila yetu na kupitia kwa Biblia na historia / mila ya kanisa.
  1. Waingereza pia lazima watambue haraka iwezekanavyo kusema – objectivity sio mungu.  Wakiendelea kuchanganya imani ya Ukristo wao na huyu ‘mungu’ wanapoteza wasikilizaji kwa kuwatoa nje ya ukweli halisi ya Mungu.  Wakiendelea kumweka na nguvu huyu ‘mungu’ yao na mkaso kali vile wanavyofanya wakati huu, matokeo yatakuwa maafa kubwa sana kwa wenyeji wa nchi ambayo siku hizi tunaita ‘nchi zinazoendelea.’

 

Bibliography

Kempson, Ruth. M.,

1977,    Semantic Theory.  Cambridge Textbooks In Linguistics.  Cambridge: Cambridge University Press

Wittgenstein, cited in Hanfling, Oswald,

1989,   Wittgenstein’s Later Philosophy. Basingstoke: Macmillan Press

 

This article can also be found, with illustration, at:

 

http://www.jim-mission.org.uk/articles/maarifa-lectur.pdf